Monday, 21 November 2016

Sinidharau

Rangi yangu inatisha, kweli sio kawaida,
Hata jua yanitisha, kujikinga kwangu shida,
Afisini nikibisha, kupata kazi pia shida,
Jina langu Alibino, ndugu yenu sinidharau.

Hilo jina kunibandika, kulikubali sikusita,
Matusi sikuyafoka, nikidhani mtasita,
Mwajifanya malaika, mababe kwenye vita,
Jina langu Alibino, ndugu yenu sinidharau.

Sisi sote tuliumbwa, kwa mfano wake mola,
Sifanani naye mbwa, ambaye mifupa anaila,
Macho yenu yatafumbwa, mkawache ukabila,
Jina langu Alibino, ndugu yenu sinidharau.

Mwili wangu mkiuona, mwauona utajiri,
Mle hadi mkanona, mgeuke makafiri,
Na magari mkavuna, kutatiza usafiri,
Jina langu Alibino, ndugu yenu sinidharau.

Leo hii ninalia, kunusuru familia,
Japokuwa tuko mia, madharau twakemia,
Tangu mwaka kendamia, yangu fora nimetia,
Jina langu Alibino, ndugu yenu sinidharau.

Serikali saidia, ni kilio tumelia,
Kila mtu katulia, kutojali letu nia,
Eti mie mpita njia, nitakufa roho pia,
Jina langu Alibino, ndugu yenu sinidharau.

Nawasihi ndugu zangu, tuikome ubaguzi,
Kisitiwe kwetu pingu, kinyume cha ukombozi,
Tuitii hata fungu, na mafunzo ya mwokozi,
Jina langu Alibino, ndugu yenu sinidharau.

myn.jpg  Mtunzi: Otieno Lawrence

                 ©2016

No comments:

Post a Comment