Thursday, 12 January 2017

Sijafa

Muda mwingi sijanena, sio eti mie bubu,
Imebidi nije tena, kwa maswala ya kutubu,
Ulichopanda utavuna, hata kama mashurubu,
Kweli mie chipukizi, niko hai sijakufa.

Nilikimya makusudi, niliona ni muhimu,
Nilikuwa sina budi, kuyatenda majukumu,
Hata hivyo nimerudi, mjulishe Allan Namu,
Kweli mie chipukizi, niko hai sijakufa.

Nimepata nyingi arafa, toka kwenu mashabiki,
Mmekosa zangu hurafa, kwa muda usiohakiki,
Nawalika kwangu ghorofa, tujadili yalohaki,
Kweli mie chipukizi, nikohai sijakufa.

Nikoshwari ninatesa, sio tu burudani,
Niko mzima kama NASA, chama kile cha upinzani,
Tawapasha vyote visa, vinapochipuka nchini,
Kweli mie chipukizi, nikohai sijakufa.

Mashabiki bwatukaji, wapendao zangu kanda,
Karibuni tunywe uji, na maziwa yaloganda,
Hapo kwake bwana Koji, afugaye wengi punda,
Kweli mie chipukizi, nikohai sijakufa.

Nimefika mwaka mpya, majaliwa yake Mola,
Ingawaje sikulipa, acha Mungu awe Mola,
Neema yake ni ya bure, hata uwe kwenye jela,
Kweli mie chipukizi, nikohai sijakufa.

myn.jpg  Na: Otieno Lawrence
                 ©2017


No comments:

Post a Comment